Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika kikao cha kielimu “Mtume wa Rehema (s.a.w.w); Chanzo cha Msukumo wa Mazungumzo ya Kimataifa” ilisisitizwa kuwa: Mtume Mtukufu (s.a.w) ni kielelezo cha maadili ya kibinadamu, mtangazaji wa umoja wa dunia na mbunifu wa ustaarabu wa Kiislamu.
Katika kikao cha kielimu chenye anuani “Mtume wa Rehema (s.a.w); Chanzo cha Msukumo wa Mazungumzo ya Kimataifa”, wasomi na wataalamu walijadili kwa kina vipengele mbalimbali vya haiba ya Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w), nafasi yake katika kujenga ustaarabu wa Kiislamu na wa kimataifa, pamoja na nafasi ya Ahlul-Bayt (a.s) katika kuimarisha na kulinda hadhi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa, kufuatia maadhimisho ya miaka 1500 ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w), kikao cha kielimu chenye mada “Mtume wa Rehema (s.a.w.w); Chanzo cha Msukumo wa Mazungumzo ya Kimataifa” kilifanyika kama sehemu ya mfululizo wa vikao vya kumtambulisha Mtume (s.a.w.w) na nafasi yake tukufu. Kikao hicho kilifanyika leo, Jumatano tarehe 7 January 2026, kwa njia ya ana kwa ana na mtandao (webinar), katika Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), kwa ushiriki wa wanazuoni wa vyuo vya dini na vyuo vikuu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na kuhutubiwa na Dk. Muhammad Legenhausen, mhadhiri wa Taasisi ya Imam Khomeini (r.a), Dk. Miftah Fauzi Rahmat, Mkuu wa Mtandao wa Shule za Mutahhari nchini Indonesia, pamoja na Hujjatul-Islam Dk. Hamed Montazeri-Moqaddam, mhadhiri wa Taasisi ya Imam Khomeini (r.a). Wahadhiri walijadili nafasi ya Mtume wa Uislamu (s.a.w) katika kukuza maadili ya kibinadamu, kuimarisha umoja wa kimataifa na kujenga ustaarabu wa Kiislamu.
Mtume wa Uislamu (s.a.w.w): Kielelezo cha mazungumzo ya kimataifa na mhimili wa umoja wa mataifa
Dk. Miftah Fauzi Rahmat, Mkuu wa Shule za Mutahhari Indonesia, katika hotuba yake alimuelezea Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) kuwa ni kielelezo cha mazungumzo ya kimataifa na mhimili wa umoja wa mataifa mbalimbali. Akitaja athari kubwa za mafundisho ya Mtume katika nchi za Asia ya Kusini Mashariki, hususan Indonesia, Malaysia na Singapore, alisema kuwa ujumbe wa Mtume (s.a.w.w) umeenezwa kwa ufanisi mkubwa katika maeneo hayo kupitia juhudi za wanazuoni wakubwa, na umeacha athari za kina katika utamaduni na maisha ya kijamii ya watu.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa tafsiri sahihi ya Qur’ani Tukufu, akieleza kuwa usahihi katika tafsiri ni jambo muhimu ili kuhakikisha kuwa mafundisho ya Mtume yanaeleweka ipasavyo, na yanaweza kuwa mwongozo wa kimaadili na kijamii kwa Waislamu na jamii nyingine.
Vilevile, aligusia maadhimisho ya Maulidi ya Mtume (s.a.w), akisema kuwa katika nchi nyingi za Kiislamu, hususan Indonesia, sherehe hizi hutumika kama fursa ya kuonesha mapenzi kwa Mtume na kuimarisha umoja wa Waislamu.
Jihadi ya kubainisha ukweli: Msingi wa ustaarabu wa Mtume wa Uislamu
Dk. Muhammad Legenhausen, mhadhiri wa Taasisi ya Imam Khomeini (r.a), katika hotuba yake alieleza kuwa jihadi ya kubainisha ukweli (Jihad al-Tabyin) ilikuwa miongoni mwa nyenzo kuu zilizotumiwa na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) katika kujenga ustaarabu. Alisema kuwa kupitia jihadi hii, Mtume aliweka misingi ya ustaarabu wa kimaadili, kitamaduni na kijamii, ambao athari zake bado zinaonekana katika jamii mbalimbali hadi leo.
Aliongeza kuwa Mtume (s.a.w.w) alijikita katika mihimili miwili mikuu: kuunda umma mmoja ulioungana na kukuza upinzani wa kitamaduni na kijamii dhidi ya dhulma, hali iliyowezesha kujengwa kwa jamii yenye uadilifu wa kijamii na mshikamano, tofauti na mifumo ya jamii zilizotangulia.
Dk. Legenhausen pia alisisitiza umuhimu wa kupambana na dhulma na ujinga, akieleza kuwa ustaarabu wa Mtume (s.a.w.w) haukuwa wa kisiasa au kiuchumi pekee, bali ulijumuisha nyanja zote za maisha ya mtu binafsi na jamii, kuanzia maadili, utamaduni, mshikamano wa kijamii hadi elimu.
Nafasi ya Ahlul-Bayt (a.s) katika kulinda hadhi ya Mtume (s.a.w.w)
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Dk. Hamed Montazeri-Moqaddam, mhadhiri wa Taasisi ya Imam Khomeini (r.a), katika hotuba yake alizungumzia nafasi ya Ahlul-Bayt (a.s) katika kulinda na kuimarisha hadhi ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w). Alibainisha kuwa baada ya kufariki kwa Mtume, juhudi na mapambano ya Ahlul-Bayt (a.s) yalikuwa na mchango mkubwa katika kudumisha nafasi ya Mtume ndani ya jamii ya Kiislamu.
Akitaja tuhuma zisizo za haki dhidi ya madhehebu ya Shia na baadhi ya tafsiri potofu kuhusu nafasi ya Ahlul-Bayt (a.s), alisema kuwa katika mtazamo wa Shia, Mtume Muhammad (s.a.w.w) daima ndiye mhimili mkuu wa dini ya Uislamu, na Ahlul-Bayt (a.s) ni walinzi na wakamilishaji wa nafasi yake.
Aliongeza kuwa baada ya kufariki kwa Mtume (s.a.w), kulikuwepo vitisho vya kitamaduni na kisiasa dhidi ya nafasi yake, lakini kwa juhudi za Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s), jina na ujumbe wa Mtume ulihifadhiwa na kuimarishwa hata katika mazingira magumu.
Katika hitimisho, alisisitiza uhusiano wa kihisia na kiroho kati ya Mtume (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt (a.s), hususan uhusiano wake na Imam Ali (a.s), akieleza kuwa uhusiano huo ulikuwa na nafasi muhimu katika kudumisha uongozi na mwongozo wa Umma wa Kiislamu.
Ikumbukwe kuwa kikao hiki cha kielimu kiliandaliwa kwa juhudi za Ofisi ya Tafiti na Utafiti wa Naibu wa Masuala ya Kielimu na Kitamaduni wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), kwa ushirikiano na Shirika la Habari la Kimataifa la ABNA pamoja na Kituo cha Mafunzo ya Muda Mfupi cha Al-Mustafa (s.a.w.w).
Your Comment